Hukumu Ya Kufuga Ndevu

Wednesday, 29 July 20150 comments

Kuachilia ndevu ni wajibu kwa wanaume kwa dalili zifuatazo:
1- Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameamuru kuziachilia. Amri hii ni ya lazima, kwani hakuna kiashirio chochote kinachoigeuza na kuipeleka katika usunnah. Na kati ya amri hizo ni neno lake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((خالفوا المشركين: وفروا اللحى، وأحفوا الشوارب))
((Kuweni kinyume na washirikina; fugeni ndevu kwa wingi na punguzeni masharubu)).[1]

Na neno lake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
((جزوا الشوارب، وأرخوا اللحى، خالفوا المجوس))
((Kateni masharubu na ziachilieni ndevu; nendeni kinyume na wanaoabudu moto)).[2]
2- Ni kwamba kuzinyoa ni sawa na kujifananisha na makafiri kama inavyoonekana katika Hadiyth mbili zilizotangulia.
3- Ni kwamba kuzinyoa ni sawa na kuubadilisha Uumbaji wa Mwenyezi Mungu na kumtii Shaytwaan asemaye:
((ولآمرنهم فليغيرن خلق الله))
«..na hakika nitawaamrisha, basi watabadili Aliyoyaumba Mwenyezi Mungu »[3]
4- Ni kwamba kuzinyoa ni sawa na kujifananisha na wanawake. Na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amewalaani wanaume wanaojifananisha na wanawake.[4]
Na kwa ajili hiyo, Shaykh wa Uislamu amesema:
“Na inaharamishwa kunyoa ndevu zake”.[5]
Ibn Hazm na wengineo, wamenukulu Ijmaa’ ya Maulamaa juu ya uharamu wa kunyoa ndevu.
Je, Inajuzu Kupunguza Ndevu Zilizozidi Mshiko Wa Kiganja?
Baadhi ya Maulamaa wamefuata mwelekeo wa kujuzu kuondosha ndevu zilizozidi mkamato wa kiganja. Wao wameshikilia Hadiyth ya Ibn ‘Umar ambaye wakati wa kuhiji au kufanya ‘Umrah, alikuwa akizikamata ndevu zake, kilichozidi alikuwa akikiondosha.
Wamesema: “Yeye ndiye mpokezi wa Hadiyth yenye kuamuru kuachilia ndevu kwa wingi, hivyo basi yeye ndiye ajuaye zaidi upokezi wake!
Katika kaulipokezi hii, wao hawana hoja yoyote kwa dalili zifuatazo:
1- Kwamba Ibn ‘Umar Allah Amridhie, alikuwa akifanya hivyo wakati anapojifungua na ihraam ya Hija au ‘Umrah, wakati wao (Maulamaa hao) wanalijuzisha hilo nyakati zote.
2- Kwamba kitendo hiki cha Ibn ‘Umar kimefahamika kutokana na yeye kuliawilisha neno Lake Subhaana:
محلقين رؤوسكم ومقصرين»  «
«…na hali mmenyoa vichwa vyenu na mmepunguza » [6]
Katika ‘amali za Hija, kichwa hunyolewa na ndevu hupunguzwa.
3- Ni kwamba Swahaba akisema au kutenda kinyume na alivyohadithia, basi kinachozingatiwa ni maneno yake na wala si ufahamu wake wala kitendo chake. Kwani mazingatio ni kile kilichorufaishwa moja kwa moja kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
Na kutokana na yaliyotangulia, lililo sawa ni wajibu wa kuachia ndevu na kutozikata kwa kuutumia ujumuishi wa amri zilizokuja katika Hadiyth sahihi kama vile: (( Fugeni kwa wingi…, ziachilieni…, zifanyeni nyingi….)) kama walivyoeleka kwa hilo jamhuri ya Maulamaa. Na Mwenyezi Mungu Ndiye Ajuaye zaidi.



([1]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (5892) na Muslim (259).
([2]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Muslim (260).
([3]) Surat An-Nisaa: 119.
([4]) Hadiyth Sahihi: Imetolewa na Al-Bukhaariy (5885) na At-Tirmidhiy (2935).
([5]) Kitabu cha “Al-Ikhtiyaaraat Al-Fiqhiyyah” cha ‘Alaau Ddiyn Al-Ba’aly (uk.10). Angalia pia kitabu cha “Al-Furu’u” cha Ibn Muflih (1/291).
([6]) Surat Al-Fath: 27
Share this article :

Post a Comment

 
Designed By Zotekali WEB Experts | Call us: +255 (0) 766 632 744
Smart Technologies in Tanzania
Copyright © 2011. MUISLAAMU | All Rights Reserved