Nguzo Za Swalah, Vitendo Vya Waajib Na Sunnah Katika Swalah

Wednesday, 29 July 20150 comments

Nguzo za Swalah ni 14: Nguzo ni zile ambazo ukiswali na ukaziacha kwa makusudi Swalah yako inabatilika, na ikiwa umeacha kwa kusahau, Swalah yako pia itakuwa haikukamilika hadi urejee kitendo chenyewe au urejee rakaa na kisha mwishoni utoe Sajdatus-Sahw. Lakini ukiwa umesahau nguzo ya Takbiyratul-Ihraam, basi itakubidi uiswali Swalah upya tokea mwanzo.

Nguzo hizo 14 ni hizi zifuatazo:
1.     Kusimama katika Swalah za Fardh kwa yule mwenye uwezo. (Wanachuoni wengine wamesema nguzo ya kwanza ni Niyah kabla ya Kusimama). Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: "Na simameni kwa ajili ya Allaah hali ya kuwa watiifu" (Al-Baqarah: 238). Na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Swali hali ya kuwa umesimama, usipoweza, basi kwa kukaa na usipoweza basi kwa kulala ubavu" (Al-Bukhaariy na Abu Daawuud).
2.      Takbira ya kuhirimia (Takbiyratul-Ihraam) kwa tamko la Allaahu Akbar kutokana na kauli ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Ufunguo wa Swalah ni kujitwaharisha, na kuifunga ni Takbira, na kuifungua ni kutoa Salaam" (Abu Daawuud na At-Tirmidhiy).
3.    Kusoma Suratul-Faatihah katika kila rakaa. Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema: "Hapana Swalah kwa ambaye hakusoma Suratul Faatihah" (Al-Bukhaariy).
4.     Kurukuu.
5.     Utulivu (Twumaaniynah) katika Rukuu.
6.     I'itidaal (hapa inaingia na kunyanyuka kutoka katika Rukuu hadi anaponyooka mtu).
7.     Utulivu katika I'Itidaal.
8.     Kusujudu.
9.     Utulivu katika kusujudu. Kutulia wakati wa kurukuu, kusujudu, kusimama, kukaa baina ya Sijdah mbili kwa msemo wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): "Kisha rukuu mpaka utulizane hali ya kurukuu, kisha nyanyuka mpaka ulingane sawa hali ya kusimama, kisha sujudu mpaka utulizane na hali umesujudu, kisha nyanyuka mpaka utulizane hali ya kuwa umekaa" (Al-Bukhaariy).
10. Kikao baina ya Sijda mbili.
11. Utulivu katika kikao baina ya Sijda mbili.
12.  Tashahhud ya mwisho.
13. Kikao katika Tashahhud ya mwisho.
14. Salaam (Kutoa Salaam) ya kwanza.
Utahakikisha unafuatanisha yote hayo kama utaratibu ulivyopangika.
Waajib Za Swalah
Ni lile ambalo ni wajibu kulifanya au kusema, inaondoka kwa kusahau na kulazimisha mwenye kuswali kusujudu sijdah mbili za kusahau. Yeyote mwenye kuacha kwa kusudi Swalah yake inabatilika ikiwa anajua uwajibu wake.
Istilahi hii inatumika kwa madhehebu ya Hanafi na Hanbali ila ma-Hanafi hawaoni kuwa mwenye kuacha wajibu kwa kusudi inabatilisha Swalah yake bali yeye amefanya madhambi anayostahiki adhabu. Ama ma-Maaliki na ma-Shaafi'y hawana kigawanyo hichi cha Waajib kwao ila wao wana nguzo na Sunnah kwa ujumla wake.
Ama hapa tutaweka yale yaliyotajwa ambayo yanaelekea kuwa na nguvu zaidi.
Kwanza kabla hatujataja mambo yenyewe, tunapaswa kujua kuwa mambo ya Waajib ni yale ambayo vilevile atakapoacha mtu kwa makusudi hubatilika Swalah yake, na atakapoacha kwa kusahau inamtosheleza yeye kusujudu Sijda mbili za kusahau 'Sujuudus-Sahw'.
Ama mambo ya Waajib ambayo yametajwa katika kitabu cha 'Swahiyhu Fiqhus-Sunnah' kwa dalili mbalimbali za Aayah na Hadiyth ni 9 kama yafuatayo:
  1. Du'aa ya ufunguzi wa Swalah 'Du'aa al-Istiftaah'.
  2. Kusema 'A'udhu biLlaahi Minash-Shaytwaan ar-Rajiym' kabla ya kusoma 'BismiLlaah ar-Ramaanir Rahiym' na 'Suratul-Faatihah'.
  3. Kusema 'Aamiyn' baada ya Suratul-Faatihah.
  4. Takbiyrah za kuhama baina ya kitendo na kitendo.
  5. Kusema 'Sami'aLlaahu liman hamidah'
  6. Kusema 'Rabbana Lakal Hamdu' katika I'itidaal.
  7. Kusema 'Subhaana Rabbiyal 'Adhwiym' wakati wa kurukuu na kusema 'Subhaana Rabbiyal A'ala' wakati wa kusujudu.
  8. Tashahhud ya kwanza.
  9. Kikao cha Tashahhud ya kwanza.
Wanachuoni wengine wametaja mambo ya Waajib ni 8 kama yafuatayo:
  1. Takbiyrah nyingine zote isiyo ile ya Ihraam.
  2. Kusema 'Sami'aLlaahu liman hamidah' kwa Imaam na mwenye kuswali peke.
  3. Kusema 'Rabbana Lakal Hamdu'.
  4. Kusema 'Subhaana Rabbiyal 'Adhwiym’ mara moja kwenye kurukuu.
  5. Kusema 'Subhaana Rabbiyal A'ala' kwenye kusujudu.
  6. Kusema 'Rabbi-Ghfir liy' kwenye kikao baina ta Sijda mbili.
  7. Tashahhud ya mwanzo.
  8. Kikao katika Tashahhud ya mwanzo.
Hizi ndizo maarufu zaidi kwa wanachuoni wengine.
Sunnah Za Swalah 
Hizi ni kauli na vitendo zinazopendeza kuletwa katika Swalah. Mwenye kufanya hayo hupata thawabu wala Swalah haibatiliki kwa kuachwa hata kwa kusudi. Wala sijdah ya kusahau hailetwi. Hapa tuna vigawanyo viwili vya Sunnah katika Swalah; Sunnah za kauli na Sunnah za vitendo.  
Sunnah Za Kauli
  1. Kisomo baada ya al-Faatihah.
  2. Dhikr nyinginezo katika Rukuu.
  3. Dhikr baada ya kusimama kutoka katika Rukuu na baada ya kusema ‘Rabbana Lakal Hamd’.
  4. Dhikr nyinginezo katika Sujuud.
  5. Du’aa baina ya Sijdah mbili.
  6. Kumswalia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Tashahhud ya kwanza na ya pili.
  7. Du’aa baada ya Tashahhud ya kwanza na ya pili.
  8. Salaam ya pili.
  9. Dhikr na du’aa mbalimbali baada ya Swalah.
Sunnah Za Vitendo
  1. Kuweka Sutrah (kizuizi mbele ya sehemu unayoswalia) katika Swalah.
  1. Kunyanyua mikono wakati wa Takbiyratul Ihraam, na wakati wa kurukuu na na wakayi wa kunyanyuka kwayo na wakati wa kuinuka kutoka katika Tashahhud ya kwanza. Na kadhalika wakati unapoinama na kuinuka.
  1. Kuweka mkono wa kuume juu ya mkono wa kushoto juu ya kifua unaposimama kuswali.
  1. Kutazama mahali pa kusujudu.
  1. Kulingana sawa mgongo unaporukuu na kutonyanyua kichwa au kukiinamisha sana, na kuweka viganja kwenye magoti mawili na huku umeviachanisha vidole vya mikono na kuachanisha viwiko visiguse mbavu au tumbo lako.
  1. Kuteremka katika Sijdah kwa mikono miwili kabla ya magoti (Wengine huona kushuka kwa magoti kabla ya mikono).
  1. Kuimakinisha paji la uso, pua na mikono (viganja viwili) kwenye ardhi pamoja na kupanua mikono isiguse mbavu zako; kuwe na uwazi wa kuweza kupita kinyama kidogo. Na viganja vyako viwe usawa wa mabega au masikio wakati uko katika kusujudu na viwiko vikiwa vimenyanyuliwa juu na vidole vya mikono vikiwa vinaelekea Qiblah. Matumbo ya vidole vya miguu yakiwa ardhini visigino vikielekea juu na hali vidole vya miguu vikielekea Qiblah.
  1. Kulilalisha guu la kushoto na kulisimamisha la kulia wakati wa kikao baina Sijdah mbili.
  1. Kurefusha kikao baina ya Sijdah mbili.
  1.  Kikao cha mapumziko baada ya kukamilisha rakaa ya kwanza na ya tatu.
  1.  Kutegemea ardhi kwa mikono wakati mtu anaponyanyuka kutoka kusujudu na kwenda kwenye rakaa nyingine.
  1.  Kukaa kikao cha Iftiraash (Kusimamisha mguu wa kulia na kukalia mguu wa kushoto) katika Tashahhud ya mwanzo. Na kukaa kikao cha Tawarruk (kusimamisha mguu wa kulia na kuipitisha mguu wa kushoto chini ya muundi wa mguu wa kulia na huku kikalio chako kimekaa juu ya ardhi).
  1.  Kuashiria kwa kidole cha shahada katika Tashahhud kuanzia mwanzo hadi mwisho bila kukishusha na huku unasoma na ukikitazama.
(Abu Maalik Kamaal Saalim, Swahiyh Fiqhus Sunnah, Mj. 1).
Hata hivyo, Shaykh Abu Bakar Jaabir al-Jazaairiy katika kitabu chake Minhaajul Muslim yeye amegawanya Sunnah za Swalah katika mafungu mawili: Zilizotiliwa mkazo kama vile Waajib na zisizotiliwa mkazo. 
Sunnah Zilizotiliwa Mkazo
  1. Kusoma Surah au Aayah katika Qur-aan baada ya Suratul Faatihah katika Swalah ya Asubuhi, rakaa mbili za mwanzo za Swalah ya Adhuhuri, Alasiri, Maghrib na 'Ishaa.
  1. Kusema ‘Sami'a Alaahu liman Hamidah’ wakati wa kuitadili na kisha Rabbaana walakal Hamd, Subhaana Rabiyal 'Adhiym wakati wa kurukuu, Subhaana Rabiyal A'alaa wakati wa kusujudu.
  1. Takbira ya kuhama.
  1. Tashahhud ya kwanza na tamko lake.
  1. Kusoma kwa uwazi katika Swalah ya kusoma kwa uwazi na kusoma kwa siri katika Swalah ya kusoma kwa siri.
  1. Kumswalia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Tashahhud ya mwisho.
Sunnah Zisizotiliwa Mkazo
1.     Du'aa ya ufunguzi.
2.     Kusoma A’udhubiLlaah.
3.     Kunyanyua mikono miwili mpaka usawa wa mabega.
4.     Kusema Aamiyn.
5.     Kurefusha kisomo katika Swalah ya Asubuhi na kupunguza katika Swalah ya Alasiri na Maghribi.
6.    Namna ya mkao, nayo ni kukalia mguu katika vikao vyote na kukalia tako katika kikao cha mwisho. Mikao ni wa Iftiraash (kukalia tumbo la mguu wa kushoto na kuunyoosha unyayo wa mguu wa kulia) na Tawarruk (kuweka tumbo la mguu wa kushoto chini ya paja la kulia na kuweka kikalio ardhini na kunyoosha unyayo wa mguu wa kulia).
7.     Kuweka mikono juu ya kifua, wa kulia juu ya wa kushoto.
8.     Du'aa katika Sijdah.
9.     Du'aa katika Tahiyyaatu.
10. Kuanzia kulia kutoa salaam.
11. Kutoa salaam ya upande wa kushoto.
 
Ingawa kuna ikhtiliaaf ya hao wanachuoni, tunapenda kuwakumbushia Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)aliyesema: "Swalini kama mlivyoniona nikiswali" (Al-Bukhaariy).
Kwa hivyo, ni juu yetu kufanya juhudi kufuata yote aliyofanya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ili tuchume thawabu nyingi zaidi. 
Share this article :

Post a Comment

 
Designed By Zotekali WEB Experts | Call us: +255 (0) 766 632 744
Smart Technologies in Tanzania
Copyright © 2011. MUISLAAMU | All Rights Reserved