Kutoa Zakaah 1

Wednesday, 29 July 20150 comments

Kutoa Zakaah ni nguzo ya tatu ya Islam. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Nguzo za Islam ni tano. Shahada kuwa hapana Mola anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Allaah, na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah, na Kusimamisha Swalah, na Kutoa Zakaah, na Kufunga mwezi wa Ramadhaan na Kuhiji Makka kwa mwenye uwezo wa kufika huko".

Kufaridhishwa kwa Zakaah ni jambo muhimu na tukufu sana kwa Waislam kwa sababu ya wingi wa faida yake na kwa ajili ya haja kubwa ya kuwepo kwa jambo hilo, kutokana na masikini na mafakiri wanaohitajia sana msaada wa ndugu zao wenye uwezo, kwani katika Kutoa Zakaah uhusiano mzuri unajengeka baina ya Waislam matajiri na Waislam masikini, na hii ni kwa sababu siku zote moyo wa mtu huelekea na kumpenda yule anayemfanyia wema na ihsani. Zakaah inasaidia pia katika kuzisafisha na kuzitakasa nyoyo.
Allaah Anasema:
خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا
"Chukuwa Sadaka katika mali zao, uwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (sadaka zao)".
At Tawba - 103
Katika kutoa Zakaah au Sadaka kunaizoesha nafsi katika kuwapendelea kheri watu wenye haja na katika kuwaonea huruma na pia kunaipatia nafsi baraka nyingi kutoka kwa Allaah Subhanahu wa Ta’ala.
Allaah ِAnasema:
وَمَا أَنفَقْتُم مِّن شَيْءٍ فَهُوَ يُخْلِفُهُ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ
"Na chochote mtakachotoa, basi Yeye Atakilipa; naye ni Mbora wa wanaoruzuku".
Saba-a - 39
Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Allaah anasema: 'Ewe mwanadamu, toa na sisi tutakupa"
Anasema Ibni Uthaimiyn:
"Kutoa Zakaah ni jambo liliofaradhishwa katika Uislam, na ni nguzo muhimu sana baada ya Shahada mbili na Swalah, na dalili ya kuwajibika kwake imo ndani ya Qurani na pia katika mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), pamoja na ijmai ya Waislam, na yeyote anayeikanusha nguzo hii anakuwa Kafir aliyertadi katika Uislam, na hukumu yake ni kutubishwa, na akitubu anasamehewa. Ama akikataa kutubu na akaendelea kuikanusha basi hukmu yake ni kuuliwa.
Ama anayeifanyia ubakhili au akapunguza katika Zakaah yake, huyo anakuwa miongoni mwa madhalimu wanaostahiki adhabu ya Allaah.
Allaah Anasema:
وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلاَ يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ. يَوْمَ يُحْمَى عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَى بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَـذَا مَا كَنَزْتُمْ لأَنفُسِكُمْ فَذُوقُواْ مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ
"Na wale wakusanyao dhahabu na fedha wala hawazitoi katika njia ya Allaah, wape habari za adhabu inyoumiza inayowangoja.
Siku (mali yao) yatakapotiwa moto katika moto wa Jahanamu, na kwa hayo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, (na huku wanaambia); "Haya ndiyo (yale mali) mliyojilimbikia (mliyojikusanyia) nafsi zenu, basi onjeni (adhabu ya) yale mliyokuwa mkikusanya."
At Tawba - 34 - 35
"Miongoni mwa faida za kutoa Zakaah anazozipata mtu katika dini yake" anaendelea kusema Sh. Ibin Uthaimiyn, "Ni kuitimiza nguzo katika nguzo za Kiislam, jambo litakalomletea mtu furaha katika dunia yake na katika akhera yake, na pia inazidi kumkaribisha mja kwa Mola wake na kumuongezea Imani, kama ilivyo katika mambo yote ya kumtii Allaah Subhanahu wa Ta’ala."
Maana ya Zakaah
Zakaah ni ile haki Aliyoifaradhisha Allaah kwa Muislam katika mali yake anayotakiwa kuwapa wanaostahiki. Neno Zakaah, katika lugha (katika kamusi ya lugha ya kiarabu) maana yake ni 'Kujitakasa', kwa sababu anayetoa Zakaah anataraji kuitakasa mali yake, nafsi yake na kupata baraka kutoka kwa Mola wake.
Allaah Anasema:
خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا
"Chukuwa Sadaka katika mali zao, uwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (sadaka zao)".
At Tawba - 103
Zakaah ni nguzo ya tatu ya Uislam iliyofaradhishwa katika Qurani tukufu na katika mafundisho ya Mtume mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na kwa sababu ya umuhimu wake, Allaah ameitaja mara themanini na mbili katika Qurani kwa kuifuatanisha pamoja na Swalah.
Imepokelewa kutoka kwa Ibni ‘Abbaas (Radhiya Allaahu anhu) kuwa amesema:
"Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipomteua Muadh bin Jabal (Radhiya Allaahu anhu) kuwa gavana wa nchi ya Yemen na kadhi wao alimwambia:
"Unakwenda katika nchi ya watu wa Ahlul Kitab, kwa hivyo (kwanza) walinganie katika shahada ya Laa ilaaha illa Allaah na kwamba mimi ni Mtume wa Allaah, wakitii juu ya hilo, wafundishe kuwa Allaah amewafaradhishia Swalah tano mchana na usiku, wakitii juu ya hilo, wafundishe kuwa Allaah amewafaradhishia Sadaka (Zakaah) za mali zao, zichukuliwe kutoka kwa matajiri wao na kurejeshewa masikini wao, na kama wakitii juu ya hilo, usije ukachukuwa mali zao zenye thamani, na uiogope dua ya aliyedhulumiwa, kwani hapana kizuizi baina yake (dua hiyo) na baina ya Allaah".
Imesimuliwa na Maimamu wote wa hadithi
Imesimuliwa pia na Attabarani kutoka kwa Aliy (Radhiya Allaahu anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Allaah amewafaradhishia matajiri wa Kiislam katika mali zao kiasi cha kuwatosha masikini wao. Na (masikini) wasingepata tabu ya njaa na mavazi isipokuwa kutokana na ubakhili wa matajiri wao. Jueni kuwa Allaah atawahesabia hesabu nzito sana na atawapa adhabu iumizayo".
Kufaradhishwa Zakaah
Zakaah imefaradhishwa wakati Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipokuwa Makka katika siku za mwanzo za Uislam, lakini hapakuwekwa Nisaab, (kiwango cha mali ambacho mtu akiwa nacho kwa muda wa mwaka analazimika kuitolea Zakaah), wala kiasi cha kulipa, isipokuwa waliachiwa Waislam wenyewe kukisia kiasi cha kutoa.
Katika mwaka wa Pili baada ya Hijra, ilifaradhishwa kiasi chake katika kila aina ya mali na kubainishwa vizuri.
Umuhimu wake (katika Qur-aan)
Katika Qurani tukufu na katika Mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), yamo mafunzo mengi yanayopendekeza Kutoa Zakaah na yanayowakemea wale wasioitoa.
Katika Qurani Allaah Anasema:
خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا
"(Ewe Mtume) Chukuwa Sadaka katika mali zao, uwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (sadaka zao)".
At Tawba - 103
Na maana yake ni "Chukuwa ewe Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) Sadaka maalum kutoka katika mali za Waislam na uwape wanaostahiki ili wenye mali 'wasafike' kutokana na uchafu wa ubakhili na tamaa, na kutokana na ubaya wa kuwanyima masikini haki zao na pia 'uwatakase' nafsi zao kwa sadaka hizo na wapate baraka za Mola wao ili waweze kupata furaha za hapa duniani na za huko akhera.
Na Akasema:
إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ. آخِذِينَ مَا آتَاهُمْ رَبُّهُمْ إِنَّهُمْ كَانُوا قَبْلَ ذَلِكَ مُحْسِنِينَ. كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ. وَبِالْأَسْحَارِ هُمْ يَسْتَغْفِرُونَ. وَفِي أَمْوَالِهِمْ حَقٌّ لِّلسَّائِلِ وَالْمَحْرُومِ
"Hakika wachamungu watakuwa katika Mabustani na chemchem.
Wanapokea aliyo wapa Mola wao .
Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema.
Walikuwa wakilala kidogo tu nyakati za usiku.
Na kabla ya alfajiri wakiomba maghfira.
Na katika mali yao ipo haki ya mwenye kuomba na asiye omba".
Adhariyaat 15-19
Katika aya hizi Allaah anatuelezea juu ya wale atakaowaingiza katika bustani Zake na chemchem, kwa sababu walipokuwa huko duniani walikuwa wenye kulala muda mfupi sana nyakati za usiku, na sehemu kubwa ya usiku, walikuwa wakiswali, na nyakati za kabla ya kuingia alfajiri walikuwa wakiomba maghfira huku wakijikurubisha kwake Subhanahu wa Ta’ala.
Walikuwa pia watu wenye kutoa katika mali zao kuwapa fakiri na maskini, wenye kuomba na wasiyo omba huku wakiwaonea huruma.
Na Allaah Akasema pia:
وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاء بَعْضٍ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلاَةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللّهَ وَرَسُولَهُ أُوْلَـئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللّهُ إِنَّ اللّهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ
"Na Waumini wanaume na Waumini wanawake wao kwa wao ni marafiki walinzi. Huamrisha mema na hukataza maovu, na hushika Sala, na hutoa Zakaah, na humtii Allaah na Mtume wake. Hao Allaah atawarehemu. Hakika Allaah ni Mtukufu Mwenye nguvu, Mwenye hikima".
At Tawba – 71
Umuhimu wake (katika Sunnah)
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Mambo matatu naapa juu yake na nakuhadithieni hadithi muihifadhi (vizuri).
Mali haipungui kwa kutoka sadaka, na mtu anapodhulumiwa akasubiri, basi Allaah humuongezea utukufu, na mtu anapojifungulia mlango wa kuombaomba, basi Allaah humfungulia mlango wa ufakiri".
Attirmidhy kutoka kwa Abi Kabsha al Anmaary (Radhiya Allaahu anhum)
Na kutoka kwa Abu Huraira (Radhiya Allaahu anhu) amesema kuwa; Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Hakika Allaah anazikubali Sadaka na anazipokea kwa mkono wake wa kuume na anailea kama mmoja wenu anavyomlea nyumbu wake mpaka tonge (anayoitoa sadaka) inafikia ukubwa wa jabali Uhud".
Ahmed - Attirmidhiy na ameisahihisha
Hadithi hii inatujulisha kuwa mtu anapotoa Zakaah au Sadaka, basi Zakaah hiyo inaingia mikononi mwa Allaah Subhanahu wa Ta’ala kwanza, kabla haijaingia mikononi mwa masikini anayepewa, ikitufahamisha jinsi gani Allaah anavyoitukuza ibada hii ya Kutoa Zakaah na jinsi anavyompenda mja wake mwenye kutoa Zakaah au Sadaka hata akaipokea kwa mikono yake Mwenyewe Subhanahu wa Ta’ala kwanza, akaizidisha jaza yake na kuifanya iwe na ukubwa wa Jabali Uhud.
Anasema Waki’i:
"Hadithi hii pia inasadikisha kauli yake Subhanahu wa Ta’ala katika Qurani pale Aliposema:
يَعْلَمُواْ أَنَّ اللّهَ هُوَ يَقْبَلُ التَّوْبَةَ عَنْ عِبَادِهِ وَيَأْخُذُ الصَّدَقَاتِ
"Je! Hawajui kwamba Allaah anapokea toba za waja Wake na kuzipokea Sadaka?"
At Tawba - 104
Na ِAliposema:
يَمْحَقُ اللّهُ الْرِّبَا وَيُرْبِي الصَّدَقَاتِ
"Allaah huyafutia (baraka mali ya) riba, na huyatia baraka (mali inayotolewa) Sadaka".
Al Baqarah - 276
Imepokelewa kuwa Anas (Radhiya Allaahu anhu) amesema:
"Mtu mmoja kutoka katika kabila la Bani Tamim alimwendea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na kumwambia:
"Ewe Mtume wa Allaah, mimi nina mali nyingi na nina jamaa wengi na wageni huja kwangu kwa wingi. Kwa hivyo nijulishe nini nifanye na vipi nitowe?"
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia:
"Utoe Zakaah kutoka katika mali yako, kwa sababu hiyo ni tohara itakayokutahirisha, na uwaendee watu wako (ndugu zako wa nasaba), na uijue haki ya masikini na ya jirani na ya muombaji".
Ahmed
Na Kutoka kwa Bibi Aisha (Radhiya Allaahu anha) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Mambo matatu naapa juu yake, Allaah hawezi kumfanya aliye na sehemu yake katika Uislam akawa sawa na yule asiye na sehemu. Na sehemu za Uislam ni tatu. Swalah, Funga na Zakaah. Na Allaah anapokuwa pamoja na mja wake hapa duniani, basi huko akhera hamuachi akawa na mwengine asiyekuwa Yeye. Na mtu anayewapenda watu hapa duniani, basi siku ya Qiyaamah Allaah Atamjaalie awe pamoja nao…."
Ahmed
Na kutoka kwa Jabir (Radhiya Allaahu anhu) amesema:
"Mtu mmoja alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam);
"Ewe Mtume wa Allaah; Unasemaje juu ya mtu anayetoa Zakaah ya mali yake?"
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
"Atakayetoa Zakaah ya mali yake, keshaiondoa shari yake".
Wasiotoa Zakaah (katika Qur-aan)
Allaah Anasema:
وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلاَ يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ. يَوْمَ يُحْمَى عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَى بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَـذَا مَا كَنَزْتُمْ لأَنفُسِكُمْ فَذُوقُواْ مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ
"Na wale wakusanyao dhahabu na fedha wala hawazitoi katika njia ya Allaah, wape habari za adhabu inyoumiza inayowangoja.
Siku (mali yao) yatakapotiwa moto katika moto wa Jahanamu, na kwa hayo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, (na huku wanaambia); "Haya ndiyo (yale mali) mliyojilimbikia (mliyojikusanyia) nafsi zenu, basi onjeni (adhabu ya) yale mliyokuwa mkikusanya."
At Tawba - 34 - 35
Na akasema:
وَلاَ يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللّهُ مِن فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُمْ بَلْ هُوَ شَرٌّ لَّهُمْ سَيُطَوَّقُونَ مَا بَخِلُواْ بِهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَلِلّهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَاللّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ
"Wala wasione wale ambao wanafanya ubakhili katika yale aliyowapa Allaah katika fadhila Zake kuwa ni bora kwao (kufanya ubakhili huko). La, ni vibaya kwao. Watafungwa kongwa (madude ya kunasa shingoni) za yale waliyoyafanyia ubakhili - siku ya Kiyama. Na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Allaah. Na Allaah ana khabari za yote mnayoyafanya."
Aali Imran - 180
Katika aya hii, Allaah amesema 'Sayutawwaquwna' na maana yake ni (Watafungwa kongwa) badala ya 'Sawfa yutawwaquna'. (Watakuja kufungwa kongwa).
Ameacha kutumia neno Sawfa’ akaiunganisha moja kwa moja kwa kusema: 'Sayutawwaquwna' kwa ajili ya kutujulisha ukaribu wa mtu kukumbana na adhabu hizo. Kwa sababu mtu akeshakufa tu Qiyaamah chake kishasimama, na kuanzia hapo mpaka siku ya Qiyaamah ataanza kukumbana na baadhi ya adhabu kutokana na yale maovu aliyoyatenda.
Wangapi wametoka majumbani mwao kwa miguu yao wenyewe, wakarudishwa wakiwa wamebebwa. Wangapi walifunga wenyewe vifungo vya suruali zao, wakaja kufunguliwa na waoshaji maiti.
Mwanadamu anapotafakari juu ya wale wanaobebwa juu ya majeneza kila siku na kupelekwa makaburini wakiacha mali zao nyingi nyuma yao, mali zitakazokuja kufaidiwa na warithi, ataona namna gani yeye alivyohangaika kuichuma mali hiyo na nani atakayekuja kufaidika nayo, na nani atakayehesabiwa juu ya mali hiyo.
Ikiwa mali imepatikana kwa njia zisizokuwa za halali au ikiwa mali hiyo haikutolewa ndani yake haki ya Allaah, basi mali hizo watasatarehe nayo warithi, na yule aliyechuma ndiye atakayeulizwa na Allaah na kuhesabiwa.
Allaah Subhanahu wa Ta’ala Akamaliza aya hii kwa kusema:
وَلِلّهِ مِيرَاثُ السَّمَاوَاتِ وَالأَرْضِ وَاللّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ
"Na urithi wa mbingu na ardhi ni wa Allaah. Na Allaah ana khabari za yote mnayoyafanya."
Na maana yake ni kuwa hata kama utawaachia mali hiyo watu wako, wao pia watakuja kufa na watakaokuja baadaye nao watakufa, na mwisho kabisa hapana atakayebaki isipokuwa Allaah Subhanahu wa Ta’ala, siku atakayozirithi mbingu na ardhi na kila kilicho juu yake.
Wasiotoa Zakaah (katika Sunnah)
Imepokelewa kutoka kwa Abu Huraira (Radhiya Allaahu anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Atakayepewa mali kisha asitoe Zakaah yake, basi mali hiyo Siku ya Qiyaamah itageuzwa kuwa joka dume lenye upara, mwenye madoa mawili machoni pake (kutokana na wingi wa sumu aliyonayo), atajizungusha katika mwili wa mtu huyo, kisha atamkaba shingoni pake huku akimwambia:
"Mimi ndiyo hazina yako uliyokuwa ukiikusanya, mimi ndiyo mali yako", kisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akaisoma aya hii:
وَلاَ يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ يَبْخَلُونَ بِمَا آتَاهُمُ اللّهُ مِن فَضْلِهِ هُوَ خَيْرًا لَّهُمْ
"Wala wasione wale ambao wanafanya ubakhili katika yale aliyowapa Allaah katika fadhila Zake kuwa ni bora kwao (kufanya ubakhili huko)".
Bukhari na Muslim
Na kutoka kwa AbdiAllaahi bin Umar bin Khattab - RadhiyAllaahu anhuma amesema kuwa; "Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Enyi watu wa Madina, mambo matano mkija mkapewa mtihani juu yake na kuteremshiwa - Najikinga kwa Allaah yasije yakakukuteni - Hautoenea uzinzi katika kaumu mpaka wakafikia kujitangazia, (isipokuwa) yatakuja kuenea kwao maradhi (aina mpya) ambayo hayajakuwepo kwa waliowatangulia, na hawatopunjwa watu katika vipimo na katika mezani isipokuwa wataletewa umasikini na shida ya kupatikana vitu, na dhulma ya ufalme. Na watakapoacha (watu) kutoka Zakaah ya mali zao, watanyimwa mvua, na lau kama si kwa ajili ya wanyama, basi isingenyesha mvua. Na watakapovunja ahadi ya Allaah na ahadi ya Mtume wake, watasalitishiwa adui asiyekuwa mwenzao achukuwe baadhi ya vilivyo mikononi mwao. Na ikiwa viongozi wao hawatahukumu kwa kitabu cha Allaah, basi vitafanywa vita vyao viwe baina yao"
Ibni Majah - Al Bazaar na Al Bayhaqi
Hukmu ya asiyetowa Zakaah
Kutoa Zakaah ni fardhi, na ni katika mambo waliyokubaliana maulamaa wote kuwa yeyote anayeikanusha fardhi hii anakuwa kesha toka katika dini akiwa ni kafiri aliyertadi, isipokuwa kama mtu huyo ni Muislam mpya, na kwa ajili hiyo husameheka kutokana na kutoelewa kwake.
Ama yule anayeacha kutoa Zakaah lakini wakati huo huo hakanushi kuwajibika kwake, huyo anapata dhambi ya kuacha kuitoa, lakini kuacha huko hakumtoi katika dini, isipokuwa ikiwa anaishi katika nchi inayohukumiwa na sheria ya Kiislam, basi anayehukumu atatakiwa aichukuwe Zakaah hiyo kwa nguvu.
Ipo hitilafu baina ya maulamaa iwapo anayeacha kutoa Zakaah atozwe gharama kwa kuacha kwake huko kwa ajili ya kumtia adabu, na gharama yenyewe ni kuchukuliwa nusu ya mali yake, na hii inatokana na hadithi iliyotolewa na Imam Ahmad na Annasaiy na Abu Daud na Al Haakim na Al Bayhaqiy kutoka kwa Bahza bin Hakim kutoka kwa baba yake kutoka kwa babu yake kuwa amesema:
"Nilimsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akisema:
"…Atakayekataa (kutoa Zakaah) tutaichukuwa (kwa nguvu, na pia tutachukua) pamoja na nusu ya mali yake haki katika haki ya Mola wetu Mtukufu na watu wa Aali Muhammad si halali kwao kuchukuwa chochote katika hiyo (Zakaah)".
Amesema Imam Ahmed kuwa isnadi ya hadithi hii ni sahihi na amesema Al Hakim kuwa hii ni hadithi sahihi.
Hata hivyo wapo baadhi ya maulamaa walioidhoofisha hadithi hii na wengine wakasema kuwa hukmu hii ilifutwa baadaye, wakiegemea baadhi ya hadithi zinazoelezea juu ya baadhi ya watu waliochelewa kulipa Zakaah na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) hakuwachukulia nusu ya mali zao.
Ama ikiwa watu watakataa kutoa Zakaah wakiwa wanaelewa kuwa ni jambo la wajibu, na ikiwa zipo nguvu za kuweza kupambana nao, basi watapigwa vita mpaka wakubali kuitoa. Na hii inatokana na hadithi iliyosimuliwa na Bukhari na Muslim kuwa AbdiAllaahi bin Umar (Radhiya Allaahu anhu) amesema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Nimeamrishwa nipambane na watu mpaka watowe shahad ya; Laa ilaaha illa Allaah Muhammadan Rasulu Allaah, na wasimamishe Swalah na watowe Zakaah. Wakishafanya hivyo, damu yao na mali zao zitakingika kwangu isipokuwa katika kulipa haki za Kiislam, na hesabu yao iko kwa Allaah".
Imeelezwa na Abu Huraira (Radhiya Allaahu anhu) kuwa; Alipofariki Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na Abubakar akawa (Khalifa), baadhi ya waarabu walikataa kutoa Zakaah, na Abubakar (Radhiya Allaahu anhu) alitayarisha jeshi akupambana nao.
Umar akasema (kumuuliza Abubakar):
"Vipi unataka kupigana vita na watu (Waislam), wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alisema:
"Nimeamrishwa nipambane na watu mpaka watowe shahada ya; Laa ilaaha illa Allaah na atakayetamka hayo itakingika kwangu mali yake na nafsi yake isipokuwa katika haki yake (anayodaiwa au kisasi kwa makosa aliyofanya), na hesabu yake iko kwa Allaah?”
Abubakar (Radhiya Allaahu anhu) akasema:
"WAllaahi nitampiga vita yeyote atakayetenganisha baina ya Swalah na Zakaah, kwa sababu Zakaah ni katika 'haki yake' (shahada hiyo). WAllaahi lau kama wataacha kunipa mbuzi mdogo (na katika riwaya nyingine 'Kamba') iliyokuwa ikilipwa wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), ningewapiga vita kwa kukataa kwao kuitoa".
Umar (Radhiya Allaahu anhu) akasema:
"WAllaahi nilipoona kuwa Allaah amemfungulia Abubakar kifua chake aamue kuwapiga vita, nikajuwa kuwa yuko katika haki".
Muslim - Abu Daud - na Attirmidhy na maimamu wengine wa hadithi.
Wanaowajibika kutowa
  • Muislam anayemiliki Niswaab, nacho ni 'Kiwango maalum cha mali kilichowekwa na sheria katika aina yoyote ile ya mali inayowajibika kuitolea Zakaah.
  • Niswaab hiyo lazima iwe ishatolewa ndani yake mahitajio ya dharura ya lazima kama vile chakula, mavazi, makazi, vyombo vya nyumbani, chombo cha usafiri na vyombo vyake vya kufanyia kazi, madeni nk.
  • Lazima kiwango hicho kiwe kimemilikiwa kwa muda wa mwaka mzima (mwaka wa Kiislam) bila kupungua katika wakati wowote ule ndani ya mwaka huo, na kama kitapungua katika wakati wowote ule kabla ya kutimia mwaka, basi hesabu nyingine mpya itaanzwa kuanzia pale kinapokamilika tena Kiwango hicho.
Amesema Imam An Nawawiy:
"Madhehebu yetu na madhehebu ya Maimam Malik na Ahmad na ya maulamaa walio wengi ni kuwa; Mali inayotolewa Zakaah kwa ajili yake, kama vile dhahabu, fedha na wanyama wa kufugwa, lazima kiwango chake kibaki kwa muda wa mwaka mzima bila kupungua. Na wakati wowote ule kitakapopungua, basi mwaka wake unakatika, na wakati wowote ule kitakapotimia tena, unaanza kuhesabiwa mwaka mwingine".
Abu Hanifa anasema:
"Kinachotakiwa ni kuwepo kwa Kiwango (Niswaab) mwanzo wa mwaka na mwisho wake, na haidhuru iwapo kitapungua katikati ya mwaka, hata kama mtu alikuwa nazo Dirham mia mbili kisha zikapotea zote katikati ya mwaka na akabakiwa na dhirham moja tu, au kama alikuwa na kondoo arubaini wakapungua na akabaki mmoja tu, kisha mwisho wa mwaka akaweza kumiliki (Dirham) mia mbili kamili au (kondoo) arubaini kamili, basi itawajibika Zakaah kwa vyote".
Masharti haya hayahusiani na Zakaah za mazao na matunda, kwa sababu vitu hivyo Zakaah yake inatolewa siku ya mavuno.
Allaah anasema:
أَثْمَرَ وَآتُواْ حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ
"Na toeni haki yake siku ya kuvuna kwake".
Al An-am – 141
Mtoto na mpungufu wa akili
Inamuwajibikia aliyekabidhiwa mali ya yatima au ya mtu mwenye upungufu wa akili kuitolea Zakaah mali hiyo ikifikia kiwango chake.
Kutoka kwa AbdiAllaahi bin Amru (Radhiya Allaahu anhu), anasema kuwa; Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Mwenye kumlea yatima mwenye mali, basi aifanyie biashara mali hiyo na asiiache mpaka ikamalizika kwa kuliwa na Sadaka (Zakaah)".
Anasema Sh. Sayed Sabeq katika Fiqhis Sunnah kuwa; Isnadi yake ina udhaifu ndani yake. Akaendelea kusema:
“Anasema Al Hafidh kuwa hadithi hii ina ushahidi kuwa ni 'Mursal' iliyorushwa moja kwa moja mpaka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) bila ya kutaja isnadi. Ama Imam Shafi ameikubali (hadithi hii) kwa sababu zipo hadithi nyingi zinazoelezea juu ya kuwajibika kwa Zakaah katika mali yoyote ile.  Anasema Imam Attirmidhiy kuwa wanavyuoni wamekhitalifiana juu ya kuwajibika kuitolea Zakaah mali ya yatima,” amemaliza kusema Sh. Sayed Sabeq.
Mwenye deni
Mwenyezi kumiliki kiwango kinachomwajibisha kutoka Zakaah, na wakati huo huo anadaiwa, kwanza anatoa kiasi cha deni analodaiwa, kisha anailipia Zakaah mali iliyobaki ikiwa bado inafikia kiwango cha kutolewa Zakaah. Ama ikiwa mali iliyobaki haifikii kiwango, basi hatoi Zakaah, kwa sababu wakati huo anahesabiwa kuwa ni mtu fakiri, na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) anasema:
"Hatoi Sadaka (Zakaah) isipokuwa mtu tajiri".
Ahmad
Na amesema:
"Ichukuliwa (mali ya Zakaah) kutoka kwa matajiri wao na kurudishiwa mafakiri wao".
Aliyefariki
Anasema Sayyid Sabeq katika Fiqhis Sunnah kuwa, katika madhehebu ya Imam Shafi na Ahmad na Abu Thour, ni kuwa mtu akifarki na akaacha deni la Zakaah, basi inawajibika katika mali yake kwanza kutolewa deni la Zakaah hata kabla ya kutimizwa wasia aloacha na kabla ya kupewa warithi.
Allaah anasema:
مِن بَعْدِ وَصِيَّةٍ يُوصِي بِهَا أَوْ دَيْنٍ
"Baada ya kutoa aliyoyausia au kulipa deni".
An Nisaa - 11
Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Deni la Allaah linastahiki zaidi kulipwa".
Na Zakaah ni deni la Allaah.
Kutoka kwa Ibni ‘Abbaas (Radhiya Allaahu anhu) kuwa amesema:
“Mtu mmoja alikuja kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
"Mama yangu amefariki na anadaiwa saumu ya mwezi mzima, je nimlipie?"
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamuuliza:
"Mama yako angelikuwa na deni ungemlipia?"
Akasema:
"Naam, ningemlipia".
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia:
"Basi deni la Allaah linastahiki zaidi kulipwa".
Bukhari na Muslim
Nia
Zakaah ni ibada, na kwa ajili hiyo Kutia Nia ni jambo muhimu kama ilivyo katika ibada yoyote ile. Na nia ni kitu cha moyoni na hakina uhusiano na ulimi, na kusudi lake ni kuwa mtu anapotoa Zakaah akusudie kuitoa kwa ajili ya Allaah.
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Hakika ya amali yoyote ni kutokana na nia, na mtu hulipwa kutokan na nia yake".
Kutowa panapowajibika
Inawajibika kuitoa Zakaah pale wakati wake unapowadia, na haijuzu kuichelewesha isipokuwa kwa dharura inayokubalika.
Kutoka kwa Bibi Aisha (Radhiya Allaahu anha) amesema kuwa; Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Haichanganyiki mali pamoja na Zakaah isipokuwa itaiangamiza", na katika riwaya nyingine;
"Inakuwa ishakuwajibikia katika mali yako kuitolea Zakaah, kisha usiitoe, kwa hivyo (mali ya) haramu (isiyotolewa Zakaah) inaiangamiza (mali ya) halali".
Shafi na Bukhari katika 'Attariykh'
Kuitanguliza
Inajuzu kuitanguliza na kuitoa kabla ya kufikia wakati wake hata kabla ya miaka miwili.
Anasema Al Shoukani katika kitabu chake 'Naylu l Awtaar';
"Maulamaa wengi kama vile Azzuhriy na Al Hassan al Basriy na Maimam Shafi na Ahmad na Abu Hanifa wamejuzisha kuitanguliza Zakaah kabla ya kufikia wakati wake".
Ama Imam Malik na Sufyan al Thouriy na baadhi nyingine ya maulamaa wameona kuwa haijuzu kuitanguliza kabla ya wakati wake, wao wameziegemea zile hadithi zinazowajibisha kutoa Zakaah baada ya kukamilika mwaka.
Anasema Ibni Rushd:
"Hitilafu iliyopo baina ya maulamaa ni kuwa - Zakaah ni Ibada au haki iliyowajibishwa kupewa masikini. Wanaosema kuwa Zakaah ni Ibada, wao wameifananisha na Swalah na wakasema kuwa haiwezekani kutolewa kabla ya kufikia wakati wake.
Ama wale wenye kuona kuwa ni haki iliyowajibika, wamejuzisha kuitoa kabla ya kufikia wakati wake ikiwa mtu mwenyewe amejitolea kufanya hivyo".
Ama Imam Shafi ameegema madai yake katika hadithi inayosema kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliwahi kuchukuwa katika mali ya Al ‘Abbaas (Radhiya Allaahu anhu) na kuitolea Zakaah kabla ya kufikia wakati wake.
Kuomba dua
Inapendeza kumuombea dua mtoaji Zakaah, pale anapoitoa.
Allaah Anasema:
خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا وَصَلِّ عَلَيْهِمْ إِنَّ صَلاَتَكَ سَكَنٌ لَّهُمْ
"Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (sadaka zao) na kuwataja kwa vizuri (mbele yangu) na uwaombee dua. Hakika kuwaombea kwako kutawapa utulivu. "
At Tawba - 103
Kutoka kwa ‘Abdullaah bin Abi Aufiy amesema:
“Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa pale anapoletewa mali ya Zakaah akisema: "Allaahumma salliy ‘alayhim". Na baba yangu siku moja alimpelekea mali ya Zakaah akasema: "Allaahumma salliy alaa aali Abi Aufiy".
Ahmad na wengineo.
Imepokelewa kutoka kwa Wail bin Hajar kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alimuombea mtu mmoja aliyeleta ngamia wa Zakaah akasema:
"Allaahumma barik fiyhi wa fiy Ibilihi". (Allaah mbariki yeye na ngamia wake)
Anasema Imam Shafi:
"Ni Sunnah kwa Imam anapopokea mali ya Zakaah kumuombea dua mtoaji kwa kumwambia: "Aajaraka Allaahu fiyma aatayta, wa baarik laka fiyma abqayta".
(Allaah akupe ujira mwema katika ulichotoa na akubarikie katika kilichobaki).
Mali inayotolewa Zakaah
  1. Dhahabu na Fedha
  2. Mazao na Matunda
  3. Mali ya Biashara
  4. Wanayama wa kufugwa
  5. Dhahabu na Fesha
Dhahabu na  Fedha
Allaah Anasema:
وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلاَ يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللّهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ. يَوْمَ يُحْمَى عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَى بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَـذَا مَا كَنَزْتُمْ لأَنفُسِكُمْ فَذُوقُواْ مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ
"Na wale wakusanyao dhahabu na fedha wala hawazitoi katika njia ya Allaah, wape habari za adhabu inayoumiza inayowangoja.
Siku (mali yao) yatakapotiwa moto katika moto wa Jahanamu, na kwa hayo vikachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao, (na huku wanaambia); "Haya ndiyo (yale mali) mliyolimbikia (mliyojikusanyia) nafsi zenu, basi onjeni (adhabu ya) yale mliyokuwa mkikusanya."
At Tawba - 34 - 35
Kwa hivyo mwenye kumiliki viwili hivyo (Dhahabu au Fedha) ikiwa ni katika mfumo wa pesa au mikufu au vipande (vinoo), ikitimia nisabu yake na kukamilisha mwaka na akawa hana deni, wala shida yoyote, anawajibika kuitolea Zakaah yake.
Wakati wa Mtume
Wakati wa Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), watu wa Bara Arabu walikuwa wakifanya biashara zao kwa njia ya kubadilishana bidhaa, na hawakuwa wakitumia pesa isipokuwa wachache sana walioweza kumiliki pesa za dhahabu na za fedha zilizokuwa zikitumika katika nchi za jirani.
Pesa zilizotengenezwa kwa dhahabu zilikuwa zikiitwa Dinari, na zilikuwa zikiletwa kutoka nchi za Warumi kama vile Byzantine na nyenginezo, na walikuwa pia wakitumia pesa zilizotengenezwa kwa fedha zilizokuwa zikiitwa Dirham na hizi zilikuwa zikitoka nchi ya Wafursi - Iran.
Kwa vile pesa hizo zilikuwa zikiwafikia zikiwa na uzito mbali mbali, na kiasi mbali mbali, nyengine ndogo ndogo na nyengine kubwa kubwa, na hazikuwa na kiasi maalum wala uzito maalum, kwa hivyo watu wa Makka hawakuwa wakizitumia kama zinavyotumiwa pesa za kawaida, bali walikuwa wakizipima na kuzipa thamani maalum waliyokubalina.
Miongoni mwa vipimo walivyokuwa wakitumia ilikuwa ratili, ambayo wakati huo ilikuwa na uzito wa wakia kumi na mbili na walikuwa pia wakitumia vipimo vya Mithqaal.
Kutokana na kipimo cha Mithqaal, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasema:
"Haitolewi Zakaah ikiwa dhahabu haikutimia Mithqaal ishirini ".
Karatasi za benki (Bank notes) zinazopigwa chapa na serikali tofauti ulimwenguni, hupigwa chapa kulingana na Dhahabu na Fedha inayomiliki serikali hizo, ama sivyo serikali yoyote masikini au yenye madeni ingelipiga chapa idadi ya noti yenye thamani kubwa kuliko dhahabu waliyo nayo na kuweza kulipa madeni yao na kujitajirisha.
Nisabu yake
Dhahabu hailipiwi kitu mpaka ifikie Nisabu yake na imilikiwe (nisabu hiyo) kwa muda wa mwaka (Mwaka wa Kiislam).
Nisabu ya dhahabu ni mithqaal 20 au gramu 92 au Tola71/2 au wakia 3. (Baadhi ya maulamaa wanasema kuwa Nisabu yake ni gramu 85 au Tola 5 au wakia 2), na hii inatokana na ugumu wa kuweza kukisia bei ya vipimo vilivyokuwa vikitumika wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na vinavyotumika wakati wetu huu. Hapana hitilafu juu ya kiwango cha Mithqaal 20 isipokuwa hitilafu ipo katika kuifasiri Mithqaal katika vipimo vya kisasa.
Inapofikia kiwango hicho, na kubaki muda wa mwaka, unaichukua na kuipeleka kuipima kwa sonara au kwa wajuzi, na baada ya kuijua thamani yake unailipia 2.5% (mbili unusu katika mia) ya thamani ya dhahabu yote.
Nisabu ya dhahabu ndiyo Nisabu ya pesa za kawaida.
Kwa mfano katika nchi ya UAE, bei ya gramu tisini na mbili ya dhahabu ni Dh. 2575/-
Kwa hivyo hicho ndicho kiwango cha kuanzia kulipia Zakaah. Na dhahabu yako inapofikia kiwango hicho unailipia Dh. 64 /- ambayo ni mbili unusu katika mia ya thamani hiyo. Dhabu inapozidi, na Zakaah yake inaongezeka.
Unailipia thamani ya dhahabu tu bila kuhesabu ujira wa mfuo au kazi ya mkono au thamani ya nakhshi zake. (Gharama za ufulishaji hazimo).
Fedha
Nisabu ya fedha ni mithqaal 140 au Tola 36 au wakia 141/2.
Ikifikia kiwango hicho na ikamilikiwa muda wa mwaka, inalipiwa moja katika arubaini au mbili unusu katika mia ya thamani yake.
Zakaah ya Deni (Mwenye kudai)
Maulamaa wameigawa deni katika hali mbili.
  1. Ikiwa anayedaiwa ni mtu tajiri au mtu muaminifu, deni hilo litachukuliwa mfano wa pesa zilizowekwa dhamana katika benki ambapo wakati wowote mtu anaweza kuzipata au ana uhakika wa kulipwa deni lake.
Katika hali hii zipo rai tatu.
  1. Ya kwanza ni kuwa mwenye kudai anatakiwa ailipie mali hiyo Zakaah yake, juu ya kuwa halazimiki kuilipia mpaka pale atakapozipata na wakati huo atailipia pamoja na Zakaah ya siku zote za nyuma.
  2. Ya pili ni kuwa analazimika kuilipia Zakaah yake kila unapotimia mwaka, kwa sababu pesa hizo zitahesabiwa mfano wa pesa zilizowekwa benki, na hii ni kwa sababu aliyekopeshwa ni mtu tajiri au muaminifu kiasi cha kuwa ana uhakika wa kulipwa au wa kuzipata pesa zake hizo wakati wowote ule anapozitaka.
  3. Rai ya tatu ni kuwa hazilipii mpaka pale atakapolipwa deni hilo, na hapo atazilipia Zakaah ya mwaka ule mmoja tu.
Anasema Sheikh Mohammad bin Uthaymiyn:
"Rai ya mwanzo, nayo ni kuilipia Zakaah ya miaka yote pale atakapozipata pesa zake ni bora zaidi na inakubalika zaidi".
  1. Ikiwa anayedaiwa ni mtu masikini au mtu asiyekuwa muaminifu, haimuwajibikii mwenye kudai kuzitolea Zakaah pesa hizo mpaka pake atakapozipata na kubaki nazo muda wa mwaka mzima kisha atazilipia Zakaah ya mwaka huo tu, ambao mali yake hiyo ilibaki kwake kama kawaida ya utoaji wa Zakaah.
Anasema Sheikh Bin Uthaimiyn:
"Haijuzu kumdai au kumlazimisha mtu masikini au kumshitaki na hatimaye kumuingiza jela na kumtenganisha na watu wake ikiwa mtu huyo hana kweli uwezo wa kulipa deni, na ikiwa mtu huyo hafanyi ujanja wa kuchelewesha makusudi, na badala yake tunatakiwa tumsitahamilie mpaka pale Allaah atakapomfariji.
Allaah Anasema:
وَاتَّقُواْ يَوْمًا تُرْجَعُونَ فِيهِ إِلَى اللّهِ ثُمَّ تُوَفَّى كُلُّ نَفْسٍ مَّا كَسَبَتْ وَهُمْ لاَ يُظْلَمُونَ
"Na kama (mkopi) ana dhiki, basi (mdai) angoje mpaka afarijike, na kama nyinyi (mnaodai mkizisamehe deni zenu) mkazifanya sadaka, basi ni bora kwenu. Ikiwa mnajua haya (basi fanyeni).
Na iogopeni Siku ambayo mtarudishwa kwa Allaah, kisha viumbe wote watalipwa kwa ukamiliyote waliyoyachuma, nao hawatadhulumiwa".
Al Baqarah - 280 - 281
Mtu akisema:
"Pesa zangu kwanini nisizidai?", Anaendelea kusema Sh. Bin Uthaimiyn,
"Tunamwamia:
Ni kweli pesa zako, lakini wewe mwenyewe ndiye uliyemkopesha pesa hizo. Pale alipokujia kutaka kukukopa ungelimtafutia udhuru wowote ule, kisha ukampa kiasi chochote cha mali ikiwa kama ni msaada tu kutoka kwako, basi yansingekukuta haya. Lakini umkopeshe na hali unajuwa kuwa mtu huyu ni masikini, kisha akishindwa kukulipa ukamshitaki, umtie jela na kumtenganisha na mke na watoto wake, jambo hilo ni haramu kabisa na haijuzu kwa Muislam kulitenda".
(Mwisho wa maneno ya Sheikh Ibni Uthaimiyn).
Zakaah ya Mapambo
Maulamaa wamekhitalifiana katika kuzitolea Zakaah dhahabu na fedha za mapambo.
Wapo waliosema kuwa dhahabu au fedha ya kujipamba inapofikia Nisabu yake lazima itolewe Zakaah yake, na hawa wameegemeza hadithi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliposema kumwambia mwanamke mmoja aliyemvisha mwanawe mkufu wa dhahabu akamwambia:
"Unailipia Zakaah yake?"
Akasema:
"La, hatuilipii"
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia:
"Huogopi Allaah akakuvalisheni mikufu ya Moto? Zilipie Zakaah yake".
Imam Ahmad
Na pia hadithi iliyosimuliwa na Bibi Aisha (Radhiya Allaahu anha) aliposema:
"Aliingia chumbani kwangu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akaniona nimevaa pete za fedha. Akaniuliza:
"Nini hiki Ewe Aisha?"
Nikamwambia:
"Nimezitengeneza ili nijipambe kwa ajili yako ewe Mtume wa Allaah".
Akasema:
"Unazilipia Zakaah yake?"
Nikasema:
"Hapana."
Akasema:
"Hiyo inatosha kwa (kukupatia adhabu ya) Moto".
Abu Daud - Addaraqutni na Al Baihaqi
Ama wale wanaosema kuwa Dhahabu ya mapambo hailipiwi Zakaah, wao wameegemeza hoja zao katika hadithi iliyosimuliwa na Al Baihaqiy inayosema:
"Jabir bin AbdiAllaah (Radhiya Allaahu anhu) aliulizwa juu ya mapambo:
"Yanatolewa Zakaah?
Akasema:
"La, hayatolewi"
Akaulizwa:
"Hata kama thamani yake itafikia Dinari elfu moja?'
Akasema:
"Zaidi" (hata kama zaidi ya thamani hiyo)
Na pia hadithi iliyomo katika Muwataa, kitabu cha Imam Malik inayosema:
"Bibi Aisha alikuwa akiwalea wana wa kaka yake mayatima na walikuwa na mapambo na hakuwa akiyatolea Zakaah.”
Atakayezichunguza hadithi hizi na zile, ataona kuwa zile zinazolazimisha kuitolea Zakaah dhahabu au fedha ya mapambo ndizo zenye nguvu zaidi na zenye uhakika zaidi kuliko zisizolazimisha - WAllaahu Ta’ala Aalam.
Zakaah ya Biashara
Hukmu yake
Wapo baadhi ya maulamaa ambao ni wachache sana wanaosema kuwa hapana dalili ya kuwa mali ya biashara inatolewa Zakaah, lakini dalili zilizomo ndani ya Qurani na Sunnah zinaleta maana kinyume na rai zao.
Allaah Anasema:
خُذْ مِنْ أَمْوَالِهِمْ صَدَقَةً تُطَهِّرُهُمْ وَتُزَكِّيهِم بِهَا وَصَلِّ عَلَيْهِمْ إِنَّ صَلاَتَكَ سَكَنٌ لَّهُمْ
"Chukua sadaka katika mali zao, uwasafishe na kuwatakasa kwa ajili ya hizo (sadaka zao) na kuwataja kwa vizuri (mbele yangu) na uwaombee dua. Hakika kuwaombea kwako kutawapa utulivu."
At Tawba - 103
Aya hii inaleta maana ya ujumla kuwa Zakaah inatakiwa itolewe kutoka katika mali zao (Matajiri), mali ya aina yoyote ile ikiwemo mali ya biashara, bila kufafanua aina ya mali hiyo.
Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:
"Ichukuliwe kutoka kwa matajiri wao na kurudishiwa mafakiri wao".
Kwa hivyo dalili hizi zinatujulisha kuwa mali yoyote ile, ikiwemo mali ya biashara, lazima itolewe Zakaah, na kwamba Zakaah hiyo ichukuliwe kutoka kwa matajiri, na bila shaka wafanya biashara ni matajiri, na kwamba irudishwe kwa masikini. Muhimu mali hiyo iwe imekifikia kile kiwango cha kutolewa Zakaah (Niswabu) na imekamilisha muda wa mwaka.
Namna ya kutoa Zakaah ya Biashara
Mwenye kumiliki mali ya biashara iliyofikia Niswabu, akishakamilisha mwaka anatakiwa ahesabu mali yake yote aliyokuwa nayo kwa ajili ya biashara. Kama ni mfaya biashara wa nyumba, basi azihesabu nyumba zake (zile tu alizozitayarisha kwa ajili ya biashara), au ardhi au vyombo vya nyumbani, magari au nguo au biashara ya aina yoyote ile. Atavihesabu vitu alivyokuwa navyo kwa ajili ya biashara pamoja na kuzihesabu pesa zote alizonazo kwa ajili ya biashara kisha atazitolea Zakaah yake, nayo ni mbili unusu katika mia au moja katika arubaini.
Atafanya hesabu hiyo bila kujali kama wakati wowote ule ndani ya mwaka ule pesa hizo zilipungua au kuongezeka.
Kumbuka
Ikumbukwe kuwa vitakavyohesabiwa ni vitu vilivyotayarishwa kwa ajili ya biashara tu.
Kwa mfano mtu anamiliki magari hata yakifikia idadi ya magari kumi au zaidi, au atataka kuuza gari lake mwenyewe kwa ajili ya kulibadilisha tu na kununua gari jengine au ardhi au nyumba au chochote kile, ikiwa anataka kuuza kwa ajili ya kutaka kununua kingine badala yake au kwa ajili ya mahitajio mengine yasiyokuwa ya kibiashara, basi mali hiyo haitolei Zakaah ya biashara, na hii ni kwa sababu nia ya kuviuza vitu hivyo si kwa ajili ya biashara.
Kumbuka pia kuwa Zakaah inatolewa kutokana na asili ya chochote kilichoongezeka kutokana mali hiyo wakati wowote ule katika mwaka. Ama kile kilichoongezeka kutokana na asili nyingine, basi mwaka wake unaanza kuhesabiwa kuanzia siku ile iliyoongezeka mali hiyo.
Kwa mfano;
Mfanya biashara alikuwa akiendela kupata faida katika biashara yake na kufikia kiasi cha Shilingi laki kumi, kisha katika mwezi wa mwisho au hata katika siku ya mwisho kabla ya kutimia mwaka, akapata faida kiasi cha Shilingi laki saba, pesa zote hizo ZITAHESABIWA pamoja na Zakaah ya biashara ya mwaka huo, kwa sababu asili yake (faida iliyopatikana) inatokana na biashara hiyo anayoitolea Zakaah.
Mfano mwingine:
Mfanya biashara alikuwa akiendelea kupata faida katika biashara yake na kufikia kiasi cha shilingi laki kumi, kisha katika mwezi wa kumi na mbili au katika siku ya mwisho au siku yoyote ile ya mwaka huo kabla ya kuingia muda wa kulipa Zakaah ya mwaka ule, mtu huyo akarithi pesa kutoka kwa jamaa yake aliyefariki kiasi cha Shilingi milioni moja.
Pesa hizo alizorithi HAZITOHESABIWA katika Zakaah ya mwaka huo, bali ataanza kuzihesabia mwaka wake mpya kuanzia siku ile alizozipata pesa hizo. Kwa sababu asili ya pesa hizo hazitokani na biashara ile anayoitolea Zakaah, bali inatokana na asili nyingine, ambayo ni urithi.
Wenye kupokea mishahara
Kwa kawaida mwenye kupokea mshahara pesa zake huongezeka na kupungua katika miezi mbali mbali. Kwa vile itakuwa vigumu kwake kuweka hesabu ya kila mwezi pale zinapokamilisha Niswabu au kuongozeka pale zinapopungua, wanavyuoni wakasema kuwa mtu huyo ataanza kuuhesabu mwaka wake kuanzia siku ile aliyoweza kutimiza Nisabu, na kuanzia mwezi huo, atakuwa akiitolea Zakaah mali yake kila anapotimiza mwaka.
Zakaah ya Mazao
Allaah amewajibisha kuyatolea Zakaah mazao Aliposema:
وَهُوَ الَّذِي أَنشَأَ جَنَّاتٍ مَّعْرُوشَاتٍ وَغَيْرَ مَعْرُوشَاتٍ وَالنَّخْلَ وَالزَّرْعَ مُخْتَلِفًا أُكُلُهُ وَالزَّيْتُونَ وَالرُّمَّانَ مُتَشَابِهًا وَغَيْرَ مُتَشَابِهٍ كُلُواْ مِن ثَمَرِهِ إِذَا أَثْمَرَ وَآتُواْ حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ
"Naye (Allaah) ndiye alyeiumba miti inayoegemezwa na isiyoegemezwa, na mitende na mimea yenye matunda mbali mbaIi, na (akaumba) mizaituni na mikomamanga inayofananana na isiyofanana. Kuleni matunda yake inapotoa matunda na toeni haki yake siku ya kuvuna kwake".
Al An-am - 141
Katika kuifasiri aya hii amesema Ibni ‘Abbaas (Radhiya Allaahu anhu):
'Haki yake, ni Zakaah yake iliyofaradhishwa".
Wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), Zakaah ya mazao ilikuwa ikitolewa katika Mahindi, Ngano, Mtama, Tende na Zabibu na wengine wakaongeza 'Mchele' na wengine wakasema kuwa Zakaah ya mazao inatolewa katika chakula chochote kile kinachoweza kubaki muda mrefu kama vile mwaka au zaidi bila kuharibika.
Matunda, hayakuwa yakitolewa Zakaah isipokuwa Tende na Zabibu. Matunda mengine hayakuwa yakitolewa Zakaah isipokuwa kama matunda hayo ni kwa ajili ya biashara, basi hapo itatolewa Zakaah ya biashara na si Zakaah ya Mazao.
Zakaah ya Mazao inatolewa siku ya kuvuna na kabla ya kuuzwa wala kuliwa na si lazima itimie mwaka.
                                           Itaendelea, Insha Allah ...
Share this article :

Post a Comment

 
Designed By Zotekali WEB Experts | Call us: +255 (0) 766 632 744
Smart Technologies in Tanzania
Copyright © 2011. MUISLAAMU | All Rights Reserved